Jumanne, 26 Novemba 2013

WAJUE WANASOKA WATANO MAHIRI ZAIDI AMBAO WANA NAFASI KUBWA YA KUTWAA UCHEZAJI BORA WA BBC 2013/2014



WASIFU WAKE: Victor Moses ni mchezaji mwenye umri wa miaka 22, ambaye kwa sasa anachezea klabu yake ya nne ya Liverpool huko England baada ya kuhama kwa mkopo kutoka klabu ya Chelsea jambo linalomweka kwenye mtihani wa kama ataweza kufurahia kiwango chake au atashindwa kudhihirisha kiwango chake.


Victor Moses ni raia wa Nigeria ambaye ana kila sifa ya kuchangia mafanikio makubwa kwenye timu. Ana kasi, ana uwezo wa kufunga magoli, ana uwezo wa kucheza nafasi tofauti uwanjani kutoka nafasi ya kiungo hadi ushambuliaji. Moses alionja ladha ya kuchezea vilabu vikubwa katika ligi kuu ya England wakati alipojiunga na Crystal Palace klabu aliyoicheza klabu hiyo uanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2010 na kufanikiwa kufunga magoli 11 katika mechi 58 alizocheza kabla ya kuhamia klabu ya Wigan Athletic. Katika miaka miwili akiwa Wigan, Victor Moses alifanikiwa kupachika wavuni magoli nane katika mechi 74 alizocheza.
Mwezi Agosti mwaka 2012, Moses alirudi tena London baada ya kununuliwa na Chelsea kutoka Wigan kwa uhamisho wa Paundi million 9. Hata hivyo baadae Kocha Jose Mourinho ambaye alirudi kufundisha Chelsea kwa mara ya pili hakumweka Moses katika orodha ya wachezaji ambao ni chaguo lake. Kwa sasa Moses amehamia Liverpool tangu mwezi Septemba mwaka huu kwa mkopo wa muda mrefu. Akiwa Liverpool makali yake yameanza kuonekana ambapo katika mechi yake ya kwanza kwenye klabu hiyo alifunga bao pale timu hiyo ilipokutana na Swansea. Moses ameshacheza mechi zaidi ya saba akiwa Liverpool na anaonekana kuwa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo walioifanya Liverpool ianze ligi kuu ya England kwa kishindo. Kwa upande wa ngazi ya kimataifa Moses anachezea timu ya taifa ya Nigeria japokuwa alishawahi kuichezea England katika timu ya vijana hadi walio chini ya miaka 21. Victor Moses ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria walioiwezesha kutwaa kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013.

Wadadisi wana maoni gani kumhusu Victor Moses?

Waandishi na wachambuzi wanamwelezea Victor Moses ni mmoja wa wachezaji ambao wamekuwa hawapangwi kuanza kila mechi kwenye klabu yake au anapocheza timu ya taifa hii ni kwa lengo la kuongeza nguvu kwa wale wanaokuwa wanacheza. Amekuwa akifurahia kila anapopewa nafasi uwanjani na hii imejidhihirisha kwa kazi yake anapokuwa uwanjani. Pamoja na uwezo, uimara na shauku yake anapokuwa uwanjani Moses ni mshambuliaji ambaye anaweza kucheza nafasi yoyote na zaidi ya hayo amekuwa akifunga magoli muhimu na kwa wakati muhimu. Mara chache amekuwa akitumiwa kama kiungo mchezeshaji lakini hufurahia zaidi anapochezeshwa kama mshumbuliaji ya nyuma.Chelsea na Nigeria zinapaswa kumshukuru Moses kwa kuzisaidia timu zao kuchukua makombe muhimu mwaka 2013. Kwa upande Chelsea Moses alifunga magoli muhimu siku ya roba fainali na nusu fainali ya ligi ya Europa ambapo baadae Chelsea ilinyakua kombe hilo. Katika timu ya taifa ya Nigeria kwenye Fainali za kombe la Mataifa ya Afrika Victor Moses alikuwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu walioiwezesha kunyakua kombe hilo na alishiriki kupiga mikwaju ya penati muhimu za mwisho. Umuhimu wake kwenye timu ya taifa unajidhirisha kwa kuteuliwa kwenye orodha ya wachezaji wanaounda kikosi cha timu hiyo japo amekosa mechi kadhaa za kufuzu kombe la dunia. Kwa ujumla kwa mwaka mzima Moses amekuwa akikabiliwa na majeraha na kufanya akose baadhi ya mechi za kimataifa kwenye timu yake ya Nigeria. Mbali na hayo kwa sasa Moses amejidhihirisha kuwa ni mmoja ya wachezaji muhimu katika kikosi cha Liverpool tangu alipojiunga na timu hiyo msimu huu wa ligi kuu ya England ambapo alifunga goli katika mechi ya kwanza wakati Liverpool ilipocheza na Swansea. Akiwa pamoja na Luis Suarez na Daniel Sturridge ambao ni washambujiaji tegemeo wa Liverpool Moses amekuwa akipangwa ili kuwasaidia kama mshambuliaji anayewatengenezea nafasi. 





Akiwa mchezaji wa timu ya Chelsea ya England kwa miaka saba, John Mikel Obi amecheza mechi 187 na kushinda makombe kadhaa, likiwemo la ubingwa wa Ligi Kuu ya England, Kombe la Mabingwa barani Ulaya na makombe manne ya chama cha mpira cha England, FA. Angaliweza kuwa mchezaji wa Manchester United, wakati huo klabu hiyo ya Old Trafford walifikiri wangemsajili mchezaji huyo kutoka klabu ya Lyn Oslo ya nchini Norway wakati huo John Mikel akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo, baada ya mvutano kuhusu suala lake, hatimaye klabu ya Chelsea ikafanikiwa kumsajili mchezaji huyo kinda mwezi Juni 2006. Tangu wakati huo, Mikel hajaweza kukengeuka kuhusu timu yake na hivyo kujijengea uwepo wake wa mara kwa mara katika kikosi cha Chelesea the Blues na kikosi cha taifa cha Nigeria-kwa kuichezea nchi yake mara 51 na kusaidia kuipatia ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu. Mikel ni mchezaji mzuri katika nafasi ya kiungo na mwenye nidhamu awapo mchezoni, na ilimchukua Mikel hadi mwezi Septemba mwaka huu kufunga bao lake la kwanza kwa timu yake ya Chelsea katika Ligi Kuu ya England, akiichezea timu hiyo mara 185, katika mechi hiyo Chelesea ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham. Labda kiwango chake cha juu kabisa alikionyesha mwaka 2012 katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich, ambapo Mikel alionyesha mchezo wa kiwango cha juu katika nafasi ya kiungo mlinzi na kusaidia timu yake kupata sare ya 1-1 baada ya dakika 120 za mchezo mkali uliomilikiwa na miamba hiyo ya Ujerumani. Chelsea waliendelea kupigana na kuingia katika hatua ya mikwaju ya penalti. Na ndipo waliposhinda na kunyakua kombe hilo, wakiwa chini ya uongozi wa kocha Roberto Dimateo. Umuhimu wa Mikel katika kikosi cha Chelsea ni kwamba mwaka jana aliongeza mkataba wa miaka mitano kuicheza klabu hiyo, hivyo kumaanisha atakuwepo Stamford Bridge hadi mwaka 2017.

Tathmini kumhusu Obi Mikel ?

Baada ya Nigeria kutwaa ubingwa mwaka 2013, huu umekuwa mwaka ambao John Mikel Obi amedhihirisha kuwa mmoja wa wachezaji mahiri kabisa barani Afrika. Hakuna mchezaji yeyote barani Afrika ambaye amepata mafanikio makubwa mwaka huu kama mchezaji huyu wa Nigeria, ambaye aliuanza msimu huu kwa mafanikio makubwa na kwenda mbele zaidi. Kufanikiwa kwa Mikel katika kusakata kandanda kumekuwa na mwelekeo mzuri lakini pia akikabiliana na changamoto kadha. Miaka mingi ya kucheza nafasi ya ulinzi katika klabu yake ya Chelsea, kumepunguza kasi yake ya kuwa mchezaji mshambuliaji katika timu yake ya taifa ya Super Eagles. Ufanisi wake katika timu ya Nigeria katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2013, kulienda mbali zaidi kuwakumbusha mashabiki mchango wake katika nafasi ya ulinzi. Katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini, alikuwa mmoja wa wachezaji wakongwe wa klabu hiyo, akiwa na umri wa miaka 25 tu na kupewa majukumu ya kuwa mshambuliaji kiungo tofauti na nafasi ya kiungo mlinzi anayochezea katika klabu yake ya Chelsea. Nigeria ilishinda Kombe la Mataifa ya Afrika, Mikel akiwa mchezaji katika mecho zote. Nigeria, Super Eagles waliwalaza Burkina Faso bao 1-0 katika mchezo wa fainali. 



Matunda ya mwanasoka Jonarthan Pitroipa kuibuka kuwa mmoja wa watakao wania tuzo ya BBC yalionekana hasa baada ya kuanza kwa michuano ya kombe la mataifa barani Afrika, ambapo Burkina Faso ilipangwa katika kundi gumu likiwa na Timu ya Zambia na Nigeria. Si tu walifanikiwa kuing’oa Chipolopolo, mabingwa watetezi, pia waliongoza kundi hilo wakiwa mbele ya Nigeria. Super Eagles ilifanya jitihada za kuishinda Burkinabe katika mchuano wa fainali, mwishowe hakuna mchezaji mwingine yeyote wa Nigeria isipokuwa Pitroipa wa Burkinafaso aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye michuano hiyo. Winga huyo kutoka klabu ya Rennes amekuwa chachu ya kufanya vizuri, akisawazisha bao dakika za mwisho katika mpambano wa ufunguzi na mchuano uliofuata akifunga bao moja na kutengeneza mawili wakati timu yake ilipokuwa ikicheza huku wakiwa kumi na kuibuka washindi wa mabao 4-0 Huo ulikuwa ushindi wa kwanza wa Stallion katika michuano ya kombe la mataifa barani Afrika tangu iliposhika nafasi ya nne mwaka 1998 timu hiyo ilipokuwa mwenyeji wa mashindano ambapo Pitroipa aliisaidia timu yake kuingia kwenye raundi ya nusu fainali alipoifungia timu yake bao 1-0 wakati wa muda wa nyongeza walipochuana na Togo. Pitroipa aliondolewa kimakosa kwa adhabu ya kadi nyekundu kwenye hatua ya nusu fainali timu yake ilipocheza na Ghana , Nyota huyo wa zamani wa Hamburg hatimae alicheza mchezo wa fainali baada ya adhabu ya kadi nyekundu kutenguliwa, hata hivyo Burkinafaso ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa goli 1-0. Hakuna mchezaji yeyote wa Burkinafaso aliyefikia hatua ya kushinda tuzo ya BBC ya mchezaji bora wa Afrika wa mpira wa miguu wa mwaka , lakini Jonathan Pitroipa anastahili. Nyota ya Pitroipa ilianza kung’aa katika kombe la mataifa ya Afrika, na zaidi fainali za mwaka huu zilizomfanya kuwa Mchezaji wa Burkinafaso wa kwanza kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo. Ni muhimu kulitilia hili maanani kwa kuwa Timu ya Burkinafaso ilisafiri mpaka Afrika kusini huku wakiwa hawana rekodi yeyote ya ushindi kwa mashindano 21 ya mataifa ya Afrika katika nchi ya kigeni. Hii ilibadilisha historia ya ushindi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Ethiopia, huku Winger huyo wa Rennes amefanikisha katika kufungwa kwa magoli matatu kati ya manne, kabla ya kuishinda Togo kwenye mchezo wa robo fainali, Burkinabe iliingia nusu fainali kwa mara ya kwanza mwaka 1998, wakati huo Pitroipa akishuhudia michuano hiyo akiwa na umri wa miaka 11.



Kwa wengi anajulikana na kukubalika kama mmoja wa Viungo bora katika kizazi cha sasa cha wanasoka.Yaya Toure ni roho ya Timu huku akitawala na kuheshimika pande zote. Mwanasoka huyu alijiunga na Klabu yake ya sasa ya Manchester City mwaka 2010 na tangu wakati huo ameshinda Taji la Ubingwa wa Ligi kuu ya Kandanda England likiwa ni taji la kwanza kwa Timu hiyo katika miaka 44,vile vile Kombe la FA,na pia ngao ya Jamii kwa Mabingwa hao wanaovalia Jezi ya Blue ya mawingu. Toure ambaye tayari ameishacheza zaidi ya mechi 109 kwenye klabu hiyo na kufunga magoli 23,yakiwemo magoli ya rekodi yatokanayo na Mipira ya adhabu,na ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika klabu hiyo. Alijunga na Manchester City akitokea Barcelona ambako alikaa kwa miaka mitatu huku akitwaa mataji kadhaa ikiwa ni pamoja na Ubingwa wa Ligi kuu ya Spain mara mbili,Ubingwa wa Ulaya mara moja,Na Kombe la Super Cup na pia taji la klabu bingwa ya Dunia.Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 vile vile amekwishatwaa Ubingwa wa Soka huko Ugiriki akiwa na Klabu ya Olympiacos,na pia Ubingwa wa Ligi kuu katika nchi yake ya asili Ivory Coast.Jambo la Kusikitisha kwa Yaya Toure ni katika medani ya kimataifa ambapo kizazi cha wanasoka kinachoaminika kuwa kizazi cha dhahabu katika soka la Ivory Coast kimeshindwa kutwaa Kombe ambalo limekuwa likitarajiwa kutoka kwao.Kwa kufungwa na Zambia mwaka 2012 katika Mechi ya Fainali ya Kombe la Mataifa yalikuwa matokeo yaliyoleta mshtuko katika Soka Barani Afrika.Hata sasa akiwa na umri wa miaka 30 Yaya Tore bado hajaonyesha dalili za kushuka kiwango ambapo ameanza vema msimu huu wa soka akiwa na Klabu yake na Manchester City ambapo hadi sasa amekwishatia nyavuni bao 7.huku akiendelea kuonyesha kiwango cha juu cha Ubora.Akiwa amekwishatwaa mara mbili taji la Mwanasoka bora wa mwaka wa Shirikisho la sokak barani Afrika CAF, Yaya Toure vile vile ni Mwanasoka pekee kutoka Barani Afrika kwenye orodha ya wachezaji 23 waliiorodheshwa kuwania tuzo ya Mwanasoka bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA mwaka huu 2013.

WADADISI WASEMAJE KUMHUSU TOURE?

Ian Hughes ,ambaye ni Mwandishi wa Habari za Michezo wa BBC anasema kuwa msimu wa mwaka 2013 unaweza ukawa si mzuri kwa Yaya Toure kwa Upande wa Mataji,lakini bado Mwanasoka wa kimataifa wa Ivory Coast,ameonyesha kasi, Nguvu,ubunifu,Magoli ya Kufunga,na hata Uongozi.

Akiwa mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya AC MILAN, soka la Pierre Emerick Aubameyang lilianza kuchomoza baada ya kujiunga na klabu ya Saint Etienne kwa mkataba wa kudumu mnamo mwaka 2011.Lakini mkataba huo ulimalizika Julai baada ya kujiunga na washindi wa pili wa Kombe la Klabu Bingwa Barani Ulaya, Borussia Dortmund , akichukua nafasi ya Mario Gotze, baada ya uhamisho wake uliotarajiwa sana kwenda Bayern Munich.Lakini mkataba wake na Les Verts ulimalizika kwa mtindo wa aina yake, kwani kalbu hiyo ilishinda taji la French League One kwa mwaka 2013, hivyo kumwezesha Aubameyang , kupata tuzo yake ya kwanza kama mchezaji wa kulipwa.Ingawa hakufunga goli katika mchezo huo, lakini aliwahi kuzifumania nyavy mara 19, katika ligi kuu ya Ufaransa , huku mchezaji wa PSG, Zlatan Ibrahmovic, akiongoza kwa mabao, na mchezaji huyo kutoka Gabon akiwa ametoa pasi nane zilizozaa mabao.Uchezaji huo mahiri ndio ulioishawishi Dortmund, kumnunua kwa kitita cha Paundi milioni 11 kwa mkataba wa miaka mitanoNa mara alijiongezea tuzo, baada ya Dortmund kulipiza kisasi cha kufungwa katika fainali ya Klabu Bingwa Barani Ulaya jijini London mnamo Mei, kwa kuwafunga mahasimu wao Bayern Munich mabao 4 -2 hivyo kutwaa taji la Supercup la ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu ya Ujerumani.Aliibuka na kuwa mchezaji wa sita kufunga mabao matatu peke yake yaani ‘Hat Trick’ katika mchezo wake wa kwanza akiwa na Dortmund ilipocheza na Ausburg na kuifunga mabao 4 – 0.Magoli yaliendelea kutiririka huku Aubameyang akijipanga vilivyo hasa kutokana na kuzifumania nyavu mara saba katika mechi 11 alizocheza katika klabu inayofundishwa na Jurgen Klopp.Wakati soka lake kwa upande wa klabu liliendelea kukua kwa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 24, mwaka 2013 ulikuwa si wa kuridhisha upande wa kimataifa.Hata hivyo, mwanga ulichomoza tena pale alipopachika ‘Hat Trick’ kwa njia ya penalty dhidi ya Niger katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia mnamo mwezi Juni, lakini huo ulikuwa ushindi pekee wa timu ya taifa ya Gabon maarufu kama ‘Panthers’ na kushika nafasi ya tatu katika kundi lao, hivyo kufuta matumaini ya kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Brazil mnako 2014.

Maoni ya wadadisi wa soka kumhusu Emerick

Mshambuliaji huyo wa Gabon alifunga ‘Hat Trick’ dhidi ya klabu ya Augsburg katika mechi ya ufunguzi ya msimu mpya na kudhiirisha moja kwa moja kwa mashabiki kwamba, alistahili kununuliwa kwa Paundi milioni 11 na kujiunga na klabu hiyo ya Ujerumani.Huo kimsingi utakuwa ulikuwa mwaka muhimu kwa mshambulijai huyo mwenye miaka 24. Mnamo mwaka 2012, alivutia katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, iliyofanyika nchini mwake na baada ye alighairi kujiunga na Tottenham Hotspur.Hivyo 2013, Aubemeyang alilazimika kudhiirisha kwamba, anaweza kufikia kiwango cha juu , na kweli alifanya hivyo .Bao lake la St Etienne, katika ushindi wa timu yake wa mabao 3 – 0 dhidi ya Bastia mnamo Januari, ulikuwa ni mwanzo wa mfululizo wa kupachika mabao ambao ulimfanya azifumanie nyavu katika mechi saba za Ligi Kuu ya Ufaransa.Aubameyang alimaliza msimu akiwa amepachika mabao 19 katika ligi, na pia alitoa pasi iliyozaa bao la ushindi katika fainali ya Kombe la Ligi la Ufaransa, baada ya St – Etienne kushinda kombe muhimu baada ya miaka thelathini.Alihusishwa na kujiunga na klabu kubwa katika majira ya jotona mengi yanasemwa kuhusu kiwango chake cha usakataji kabumbu, na kwamba, Borussia Dortmund, timu ambayo iliifunga Real Madrid ili kufikia fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya, ilipambana vilivyo kupata saini ya mwanandinga huyo.Inawezekana Aubameyang hapangwi katika kikosi kinachoanza pale timu yake inapocheza kwa sasa, lakini Jurgen Klopp, mpishi wa mafanikio ya Dortmund, anasema tayari ameonesha mafanikio makubwa na kuvutia, katika moja ya vilabu vyenye kipaji Barani Ulaya.Moja ya mafanikio hayo ni pamoja na kufanikiwa kukimbia muda wa haraka zaidi kwa mita thelathini kuliko bingwa wa mbio za mita 100 duniani Usain Bolt.Licha ya juhudi kubwa za Aubameyang, timu ya taifa ya Gabon imeshindwa kuonesha cheche kwa mwaka 2013, lakini kwa upande wa klabu umekuwa ni mwaka wa mafanikio kwa mshambuliaji huyo.Na hivyo basi nitampigia kura kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika wa BBC kwa mwaka 2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni