MJUE KITWANA MANARA
Kitwana Manara maarufu kama ( POPAT ) ni
mchezaji ambaye hata sahaurika katika rekodi ya wachezaji waliowahi kuichezea
Klabu ya Yanga katika miaka ya 60 hadi 80
Alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga
walioiwezesha timu hiyo kuwa ya kwanza nchini kufuzu kucheza robo fainali ya
michuano ya klabu bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970.
Katika hatua zote hizo mbili, Yanga ilitolewa
na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo katika robo fainali ya mwaka 1969,
iliondoshwa kwa njia ya kura ya shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya
bao 1-1.
Katika robo fainali ya pili mwaka 1970, Yanga
ilikutana tena na Asante Kotoko, ambapo katika mechi ya awali, zilitoka sare ya
bao 1-1 na katika mechi ya marudiano, hazikufungana.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane
katika muda wa nyongeza, lakini kutokana na giza kutanda uwanjani, mechi
ilivunjika dakika ya 19 na hivyo kuhamishiwa kwenye uwanja huru wa mjini Addis
Ababa, Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya tatu, Yanga ilikubali
kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Asante Kotoko na kutolewa kwenye hatua
hiyo. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa chini ya Victor Stanculescu kutoka
Romania.
Manara pia alikuwa miongoni mwa wachezaji
walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza
michezo ya All Africa Games mwaka 1973 na
kutinga nusu fainali, ambapo ilitolewa na Algeria baada ya kuchapwa mabao 2-1.
“Kwa kweli kama ni rekodi ya mwanasoka
aliyecheza soka kwa miaka mingi hapa nchini na kwa nafasi mbili tofauti, hakuna
anayeweza kuifikia rekodi yangu,”alisema. “Mimi nilianza kuichezea timu ya
taifa kuanzia kwenye michuano ya Gossage hadi ilipobadilishwa jina na kuitwa
Chalenji.”
Akizungumza na Official Website ya Klabu Young
Africans Sports Club ( www,youngafricans.co.tz, )hivi karibuni kuhusu mafanikio
ya soka katika miaka ya 50 ya Uhuru, Manara alisema Tanzania imepiga hatua
kubwa na kupata mafanikio ya kuridhisha.
Akitoa mfano, Manara alisema japokuwa
kiwango cha uchezaji soka miaka ya nyuma kilikuwa juu ikilinganishwa na
hivi sasa, kuwepo kwa vifaa vingi vya michezo na viwanja vya kisasa vya
kuchezea mchezo huo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Alisema miaka ya nyuma, vifaa vya michezo
vilikuwa vichache na viwanja vilivyotumika kuchezea mchezo huo vilikuwa vya
kawaida.
“Hivi sasa, timu yetu ya taifa imepata udhamini
mkubwa, wachezaji wanalipwa vizuri, klabu zinamiliki viwanja vyao vya kuchezea
soka, haya yote kwangu mimi ni mafanikio makubwa,”alisema.
Manara pia alieleza kufurahishwa kwake kuona
Taifa Stars ikipata maandalizi kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za mataifa ya
Ulaya huku ikipatiwa huduma zote muhimu.
Alisema miaka ya nyuma, ilikuwa vigumu kwa
mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo kila ilipocheza ama
kuhamasika na kuvaa fulana zenye rangi ya bendera ya taifa.
Manara alisema pia kuwa, soka inayochezwa hivi
sasa ni ya kasi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakini baadhi ya vitu
vinavyofanywa na wanasoka maarufu duniani kama vile Lionel Messi wa Barcelona
ya Hispania si vigeni kwa Tanzania.
Aliwataja baadhi ya wanasoka wa zamani
waliokuwa na uwezo wa kucheza na mpira wanavyotaka, kupiga chenga na kupangua
idadi kubwa ya mabeki kwa wakati mmoja kuwa ni pamoja na Mbwana Abushiri, Emily
Kondo, Arthur Mambeta, Sunday Manara na Abdalla Kibadeni.
Alisema uwezo wa wanasoka hao haukuweza
kutambulika kimataifa kutokana na kutokuwepo kwa vyombo vingi vya habari kwa
ajili ya kuwatangaza. Alisema vyombo vilivyokuwepo wakati huo kama vile
magazeti, vilikuwa vichache na teknolojia ya televisheni haikuwepo.
Manara alisema Tanzania ni nchi pekee kwa nchi
za ukanda wa Afrika Mashariki iliyoweza kutoa wanasoka wengi nyota,
ikilinganishwa na nchi za Kenya na Uganda.
Akizungumzia uongozi wa soka nchini, Manara
alisema viongozi wa zamani wa klabu hawakuwa na elimu kubwa, lakini waliweza
kubuni vitu vingi na kuziletea mafanikio makubwa klabu zao. “Asikudanganye mtu,
mafanikio ya Taifa Stars yanapaswa kuanzia klabuni. Kukiwa na migogoro kwenye
klabu hizo mbili, timu yetu ya taifa nayo itakuwa mbovu,”alisema.
Manara ameupongeza uongozi wa sasa wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuleta mageuzi makubwa katika mchezo huo,
ikiwa ni pamoja na kurejesha nidhamu kwa viongozi na kuleta utendaji mzuri.
“Kwa kweli mabadiliko katika uongozi wa chama
cha soka yameonekana. Zamani pale uwanja wa Karume kulikuwa na jengo dogo tu
kwa ajili ya ofisi za chama, lakini hivi sasa kuna ghorofa na uwanja wa kisasa
wa mazoezi. Haya ni mafanikio makubwa,”alisema.
“Serikali nayo imejitahidi sana kutuletea
makocha wa kigeni kwa ajili ya timu ya taifa na wachezaji wamekuwa wakihamasika
kuichezea. Haya nayo ni mafanikio makubwa,”aliongeza.
Manara alimmwagia sifa kemkem Rais wa TFF,
Leodegar Tenga kuwa ni kiongoni pekee
aliyeleta mageuzi makubwa katika uongozi wa
soka nchini na pia kuleta heshima kwa chama hicho.
Alisema nidhamu ndani ya shirikisho hilo
imekuwa kubwa na kamati zimeachwa zifanyekazi zake kwa uhuru mkubwa bila ya
kuingiliwa.
“Kwa kweli hajatokea kiongozi aliyeleta amani
na utulivu katika chama cha soka kama Tenga. Waswahili wanasema, mnyonge
mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Tenga anastahili pongezi,”alisema.
Hata hivyo, Manara alisema wapo viongozi
wengine wa chama hicho waliofanya vizuri huko nyuma, lakini hakuna anayeweza
kufikia rekodi ya Tenga.
Manara amelitaka shirikisho hilo kufanya
jitihada zaidi liwe na uwanja wake wa kuchezea soka kwa ajili ya kuongeza
mapato yake, tofauti na ilivyo sasa, ambapo linategemea zaidi mgawo wa mechi za
ligi kuu na za kimataifa.
Ameiomba serikali ifikirie kupunguza kodi
kwenye vifaa vya michezo ili vijana wengi zaidi waweze kumudu kuvinunua na
hivyo kuongeza hamasa kwao ya kushiriki katika mchezo huo.
Manara pia ametoa mwito kwa viongozi wa klabu
na vyama vya soka, wawe wabunifu wa vyanzo vya mapato na uendeshaji wa mchezo
huo kisasa zaidi badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.
"Umefika wakati sasa, lazima kuwe na
mabadiliko. Kiongozi anapochaguliwa kuongoza klabu, awe mtendaji wa kazi
anayeipenda klabu yake. Asiwe mtu wa kuweka mbele mapato,"alisema.
Amewataka wanasoka wa Tanzania waone thamani ya
kucheza soka kwa sababu mpira ni ajira na mchezaji anaweza kulipwa mamilioni ya
shilingi kwa ajili ya usajili pekee.
“Kama mchezaji anaweza kulipwa milioni 60 kwa
msimu, anapaswa kuuheshimu mpira katika maisha yake kwa sababu ndiyo ajira
yake,”aliongeza.
Amewataka viongozi wa klabu kuzithamini timu za
vijana kwa vile ndizo chimbuko la wanasoka. Alisema timu hizo zinapaswa kupewa
huduma zote muhimu kama ilivyo kwa timu za wakubwa ikiwa ni pamoja na kuzipatia
usafiri wa uhakika.
Manara alianza kucheza soka katika timu za
mitaani za Sambwisi, Young Boys, Cosmo, TPC ya Arusha, Feisal na baadaye Yanga
na Pan African. Alistaafu rasmi kucheza soka mwaka 1983 akiwa Yanga, ambayo
katika miaka miwili ya mwisho, aliifundisha akiwa kocha mchezaji.
Akitoa mfano, alisema viongozi wa Yanga
waliweza kununua nyumba mtaa wa Mafia kwa sh. milioni 11 kutokana na mapato ya
sh. milioni 20 katika mechi kati yao na Abaluya ya Kenya na siku hiyo wachezaji
hawakulipwa hata nauli.
“Hivyo utaona kuwa, uongozi wa zamani ulikuwa
wa kujitolea zaidi na viongozi walihakikisha kila mchezaji anatafutiwa kazi na
walicheza kwa moyo kwa sababu walikuwa wanachama wa klabu wanazochezea hivyo
ilikuwa vigumu kuzihujumu,”alisema.
Alisema viongozi wa sasa wa klabu wana elimu
kubwa, lakini wanakosa ubunifu na mashabiki wa klabu kongwe za Simba na Yanga
wamekosa imani kwa viongozi wao, hasa timu zao zinapofungwa katika mechi
muhimu.
Mkongwe huyo alisema ubunifu wa viongozi wa
zamani ulianza kutoweka miaka ya 1976, ambapo klabu za Simba na Yanga zilianza
kutawaliwa na migogoro mingi, iliyosababisha zigawanyike.
Alisema migogoro hiyo ndiyo iliyosababisha
klabu ya Yanga kugawanyika na kuzaliwa Pan African na ile ya Simba nayo
kugawanyika na kuzaliwa Nyota Nyekundu.
UNAWAKUMBUKA HAWA JAMAA
Kutoka kushoto mwenye mpira ni Zamoyoni Mogella wa Simba Sports, aliyejulikana kwa jina la Golden Boy, kushoto kwake ni mlinzi wa Yanga Yusuf Bana na kati kati ni Athuman China wa Yanga pia. ilikuwa balaaaa wakati huo